Friday, February 17, 2017

VYAKULA MAARUFU KWA KUZUIA UVIMBE MWILINI


Vyanzo vinavyoweza kusababisha mlipuko wowote wa uvimbe mwilini na magonjwa mengini ya aina hiyo ni vingi, kutokana na aina ya vyakula tunavyokula, mazingira tunayoishi na hata msongo wa mawazo unaosababishwa na kazi tunazozifanya.

Kwa kawaida mwili umeumbwa kujikinga  wenyewe na kuwa na uwezo wa kupambana na kuzuia maambukizi ya maradhi na milipuko kama hiyo. Ili mwili uwe na uwezo huo, unahitaji uupe uwezo kwa kula vyakula vinavyoongeza kinga mwilini, hasa kinga ya kuzuia uvimbe, miongoni mwa hivyo ni pamoja na hivi vifuatavyo:

MAHARAGE
Jamii yote ya maharage, ikiwemo na soya, inaaminika kuwa na kiasi kingi cha protini na virutubisho vingine vingi vinavyohitajika mwilini kuzuia magonjwa ya mlipuko na uvimbe. Pia vyakula hivi vinafaa kwa wagonjwa wa moyo.

SAMAKI NA MAFUTA YAKE
Ulaji wa samaki, hasa aina ya jodari, ni muhimu sana, kwani samaki hawa wana kiwango kingi cha virutubisho aina Omega-3 na 6. Ukiweza, pendelea kula samaki kila mara katika mlo wako wa kila siku. Halikadhalika, utumiaji wa mafuta ya samaki, kiasi cha kijiko kimoja au viwili kwa siku ni muhimu ili kuimarisha kinga ya mwili.

VIUNGO
Katika mlo wako wa kila siku, usipuuzie viungo vya mboga vyenye asili ya miti, kama vile bizari, mdalasini, tangawizi na hiriki. Miti hii ina kiwango kikubwa cha virutubisho vyenye uwezo wa kupambana na kutoa kinga dhidi ya magonjwa ya uvimbe. Hivyo hakikisha kwenye mapishi yako, unaangalia namna ya kuchanganya viungo hivi.

VIAZI VITAMU
Viazi vitamu vina kiwango kikubwa pia cha virutubisho vyenye uwezo wa kung’arisha ngozi, kuimarisha kinga ya mwili na pia afya ya moyo. Kwa upande wa kuzuia magonjwa ya uvimbe, viazi pia vimetajwa kuwa na uwezo mkubwa sana. Mbali ya viazi, pia hata maboga na karoti nazo zina virutubisho vingi vya kuimarisha kinga ya mwili.

CHAI
Unaweza kupamba na magonjwa ya uvimbe na kuupa mwili wako kinga ya mwili dhidi ya magonjwa hayo hata kwa kunywa chai, hasa ya majani ya kijani (green tea), ambayo utafiti wa kitabibu unaonesha kuwa na kiwango kingi cha virutubisho vya kuongeza kinga ya mwili.

Kwa ujumla, ni vyema kuwa na kawaida ya kula vyakula asili vya aina mbalimbali na bila kusahau mboga za majani ya aina mbalimbali pamoja na matunda ili kujenga kinga ya mwili imara ambayo itakuwa tayari kupambana, siyo tu na magonjwa ya uvimbe mwilini, bali hata magonjwa mengine hatari.

Thursday, February 16, 2017

Lishe bora kwa maisha ya kila siku.


Inajulikana kabisa kuwa nyumba imara hujengwa kwa mchanganyiko wa vitu vingi. Nyumba hii huonekana nzuri na yenye kupendeza wakati wote na pia haimomonyoki kirahisi wakati wa mvua au upepo mkali. Nyumba imara hujengwa kwa mchanganyiko kama wa cementi, mchanga, kokoto, nondo n.k. mchanganyiko huu huwa katika kiwango sahihi, hii ni kwamba kuna kiasi au uwiano sahihi katika mchanganyiko huu. Kimojawapo kati ya hivi kikipelea au kuwa katika kiasi pungufu basi nyumba haitakuwa imara, vilevile kimojawapo kikizidi basi nyumba haitakuwa imara pia. Hivyo nyumba ili iwe imara ni lazima mchanganyiko huu uwe katika uwiano ulio sahihi.

Mpaka hapo swali linakujia, je mwili wako unajengwa na nini? je kuna uhitaji wa uwiano sahihi?
Mwili wa binadamu hujengwa kwa chakula. Chakula hicho ni lazima kiwe chakula bora au mlo kamili. Mlo kamili unajumuisha makundi matano ya vyakula ambayo ni: nafaka, mizizi na ndizi, kundi la pili: vyakula vyenye jamii ya kunde na vyenye asili ya wanyama, kundi la tatu: mbogamboga, kundi la nne: matunda, kundi la tano: mafuta na sukari.

Mwili unahitaji chakula chenye mchanganyiko wa makundi haya ya chakula ili kuwa na afya bora na iliyo imara kama inavyolinganishwa na nyumba imara. Inajulikana kuwa mchanga ukizidi katika tofali nyumba itamomonyoka nakuanguka au cementi ikipungua pia nyumba itamomonyoka na kuanguka. Hii ni sawa na ulaji kwa binadamu, chakula kikiwa hakina au kina kiwango kidogo cha baadhi ya makundi ya chakula yaliyotajwa hapo juu lazima mwili utakuwa dhoofu, hata makuzi yake hayatakuwa mazuri. Magonjwa yatokanayo na utapiamlo ndio chanzo kikuu cha mwili kuwa na afya mbaya. utapia mlo hutokana na lishe duni au lishe iliyozidi.

Lishe duni ni hali ya mwili kukosa baadhi ya virutubishi vinavyohitajika mwilini, kama vile protini, wanga, mafuta, vitamini na madini. Mwili ukikosa baadhi ya virutubishi hivi hushindwa kufanya kazi zake za kimebotali vizuri na kusababisha madhara mengine mengi. Vilevile mwili ukiwa na lishe iliyozidi husababisha madhara makubwa hii inatokana na kubadilika kwa baadhi ya kazi za seli na ogani mbalimbali mwilini.

Magonjwa ya utapia mlo ni kama vile: kwashakoo, marasmasi, marasmasi na kwashakoo, upungufu wa damu (Iron Deficiency Anaemia), tatizo la ukosefu wa vitamini C, tatizo la Ukosefu wa vitamini A, tatizo la ukosefu wa madini Joto, na magonjwa yatokanayo na lishe iliyozidi ni kama kisukari, presha, magonjwa ya moyo ambayo ndio tatizo kubwa linalowakumba hasa matajiri wanaojikita zaidi katika vyakula vyenye mafuta mengi na sukari.                                                 
                                          
  Kundi la chakula, chanzo chake, virutubishi vyake, na kazi yake mwilini  

1. Nafaka, Mizizi na Ndizi

  • mchele, mahindi, mtama, ulezi, ngano, uwele, viazi vikuu, viazi vitamu, mihogo, magimbi, viazi mviringo, na Ndizi
  • Virutubishi: Wanga
  • Huupatia mwili nguvu za kuweza kufanya kazi


2.Vyakula vya aina ya mikunde na vyenye asili ya wanyama

  • Maharage, kunde, mbaazi, soya, karanga,njegere, njugu mawe,dengu, choroko, asili ya wanyama ni: nyama, mayai, samaki, dagaa, kumbikumbi, senene, maziwa na nzige.
  • Virutubishi: Protini
  • Hujenga mwili. Huwezesha mwili kutengeneza seli nyingine.


3.Mboga-mboga

  • mchicha, majani ya kunde, majani ya maboga, kisamvu, matembele, spinachi, mgagani, mlenda, mnavu, mchunga, karoti, pilipili hoho, nyanya chungu, biringanya, bamia, kabichi, figiri, sukuma wiki na chainizi.
  • Virutubishi: Vitamini na Madini
  •  Huupa mwili kinga imara dhidi ya maradhi mbalimbali.


4.Matunda

  • mapera, maembe, machungwa, papai, nanasi, zambarau, dhabibu, mapesheni, machenza, ubuyu, ukwaju, limao
  • Virutubishi: vitamini na madini
  •  Huupa mwili kinga dhidi ya maradhi.
  • Husaidia kwa baadhi ya virutubishi kutumika kwa ufasaha zaidi mwilini.


5.Mafuta na Sukari

  • mafuta ya kupikia, ufuta, karanga, mbegu za alizeti, siagi, samli, nyama yenye mafuta, sukari ni: asali, miwa, vyakula vinavyotengenezwa kwa sukari nyingi kama jamu, keki, n.k
  • virutubishi: mafuta
  • Huupa mwili nguvu.
  • Husaidia ufyonzwaji wa vitamini A,D,E na K.


Maji???????
Maji hayakuwekwa kwenye kundi lolote la chakula kwa sababu hayana virutubishi. Ni muhimu kunywa maji safi na salama kwani yanarahisisha umeng'enyaji wa chakula, kusafirisha virutubishi na kutoa uchafu ambao hutengenezwa mwilini wakati mwili unafanya kazi zake. Asilimia kubwa ya mwili ni maji hivyo ni vyema kunywa maji mara kwa mara ili kuwa na afya bora.

Kumbuka:
ni vema kula vyakula vyenye mchanganyiko wa kila kundi la chakula ili mwili uwe na afya nzuri, na kutopatwa na maradhi mara kwa mara, pia kunywa maji safi na salama wakati wote unapohitaji.